Monday, January 7, 2013

HISTORIA FUPI YA MAREHEMU SAJUKI NA CHANZO CHA MAUTI YAKE...

KAMA ilivyo kawaida ya maisha ya binadamu, kuna kupanda na kushuka. Katika maisha ya aliyekuwa staa wa filamu za Kibongo, marehemu Juma Kilowoko ‘Sajuki’ alipanda na kushuka na alipitia katika raha na shida ambazo ndizo zilikuwa nyingi.

HISTORIA
Sajuki alizaliwa Aprili 4, 1986 mkoani Songea na kupata elimu ya msingi katika Shule ya Mfanyakazi, Manispaa ya Songea kuanzia mwaka 1995 hadi 2001.

Mwaka 2002 alijiunga na shule ya Sekondari ya Jeshi Ruhuwiko ambayo nayo ipo Manispaa ya Songea hadi alipohitimu kidato cha nne mwaka 2005.

MISHEMISHE ZA KUCHOMOKA KIMASHA DAR
Mwishoni mwa mwaka 2005, Sajuki aliingia rasmi jijini Dar es Salaam na kuanza kwa kufanya biashara ndogondogo ambapo mwaka huohuo alianza kusaga soli akiomba kuingia kwenye Kundi la Sanaa la Kaole.

Pamoja na changamoto kibao lakini hakukata tamaa. Alifanikiwa na akaonesha kipaji kwenye michezo mbalimbali iliyokuwa ikirushwa katika Kituo cha Runinga cha TVT (kwa sasa TBC1).

AINGIA KWENYE FILAMU
Baada ya kuonekana kwenye michezo kadhaa akiwa Kaole, Sajuki aliingia kwenye uchezaji wa filamu ambapo ya kwanza kuonekana ni ile ya Revenge aliyoshirikishwa na mwigizaji Vincent Kigosi ‘Ray’.

Hakuishia hapo, baada ya filamu hiyo aliendelea kusaka mingo za filamu ambapo ya pili ni ile ya Victoria. Kabla hajakaa vizuri akakutana na mwigizaji Deogratius Shija ambaye alimpa shavu kwenye Two Brothers na nyingine nyingi.

Safari ikaanza, zikafuata nyingine za Mboni Yangu, Shetani wa Fedha, Vita, The Killer, Round, Kozo Pata, Mchanga, Brifcase na ya mwisho ni Kivuli aliyocheza akiwa anaumwa.

SHIJA AMKUTANISHA NA WASTARA
Mwaka 2008, Shija aliwakutanisha Sajuki na mkewe Wastara kwenye filamu ya Two Brothers ambapo huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa uhusiano wao mpaka kuja kuoana.

Mwaka 2009, wawili hao walifunga ndoa ikiwa ni miezi kadhaa tangu Wastara akatwe mguu kutokana na ajali ya pikipiki waliyoipata wakiwa pamoja wakati wa uchumba.
Siyo siri, ndoa yao imekuwa mfano wa kuigwa na jamii pamoja na mastaa wenzao kwani walikuwa wanapendana kupindukia.

KUUGUA
Sajuki alianza kuugua tangu mwaka 2011 ambapo alitibiwa katika Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam. Baada ya hali kuwa mbaya alihamishiwa Muhimbili na kugundulika kuwa alikuwa na uvimbe tumboni.

Baada ya uchunguzi huo, mwaka 2012 alipelekwa India kwa ajili ya matibabu ambapo alifanyiwa uchunguzi upya na kugundulika kuwa ana ugonjwa wa saratani ya ngozi, uvimbe tumboni na upungufu wa damu.

Alipewa dawa za kutumia kwa miezi kadhaa na kuambiwa arejee tena lakini mauti yamemkuta akiwa kwenye maandalizi ya kurudi India.

Sajuki alifariki Januari 2, mwaka huu katika Hospitali ya Muhimbili na ameacha mjane na mtoto mmoja mwenye umri wa miezi kumi aitwaye Farheen.

Credit:GPL


www.jonasakamimi@gmail

No comments:

Post a Comment