HOME

Wednesday, November 14, 2012

Uozo Mkubwa Waibuka Bongo Movies-JB na Wenzako Mmewakosea Sana Wenzenu


HABARI zenu wapenzi wasomaji wa safu hii pendwa ya Michano ambayo inalenga kufundisha au kumbadilisha mtu hususan wasanii ambao tangu kale inaaminika kuwa ni kioo cha jamii. Tunawekana sawa kiroho safi.
Leo nataka kuwazungumzia Bongo Movie na maruweruwe yao. Amani imetoweka ndani ya klabu hiyo, sina haja ya kuelezea hali halisi ilivyo kwa sasa lakini kwa kifupi, kimenuka!
Mwenyekiti wa Bongo Movie unayemaliza muda wako, Jacob Steven ‘JB’ na wenzako tisa, hamkuwatendea haki wenzenu na mnatakiwa kuwaomba radhi kwa lengo la kuifanya Bongo Movie iendelee kuwa hai.
Nayasema haya baada ya kufanya uchunguzi wangu kutaka kujua nini hasa kinachosababisha amani inakosekana ndani ya Bongo Movie ambapo nimegundua uozo mkubwa.
Kama ulikuwa hujui, vinara wa klabu hiyo kuanzia kwa Mwenyekiti JB, Vicent Kigosi ‘Ray,’ Hartman Mbilinyi, Issa Musa ‘Cloud’, Single Mtambalike ‘Rich’, Steven Mengele ‘Steve Nyerere’, William Mtitu na Jacqueline Wolper wapo kwa ajili ya masilahi yao binafsi na ndiyo maana sasa wamekuja na kitu kipya, Bongo Unit.
Yaani inafahamika kuwa kuna klabu inaitwa Bongo Movie lakini kumesajiliwa tena klabu mpya iitwayo Bongo Unit, ikiwa na wasanii kumi niliowataja hapo juu. Klabu ndani ya klabu, taasisi ndani ya taasisi! Kwa nini? Kuna nini kilichojificha hapa?
Kwa mujibu wa habari za kuaminika, niliowataja ni wamiliki wakuu wa klabu kwa maana hiyo mmoja akifa basi familia yake inarithi haki za ndugu yao, ni wizi na unyonyaji wa hali juu ndiyo maana sasa hivi dhambi mliyofanya inawarudia.
Haiwezekani muende kusajili taasisi kubwa kama hiyo bila ya kuwaambia ukweli wenzenu huku mkiwaacha wakijua kuwa Bongo Movie ni ya wote, msingedhulumiana hizo fedha siri hii ingevujaje?
Inadaiwa kuwa baada ya viongozi wajuu kudhulumiana fedha ambazo wasanii wengi wa Bongo Movie walikuwa wakidhani kuwa kila kinachoingia kinawekwa benki, jukumu ambalo Ray ndiye mhusika kumbe hao wachache niliowataja walikuwa wakigawana ndipo Issa Musa ‘Cloud’ alipoamua kujikosha kwa wasanii wengine na kuwaambia kuwa mtafanyaje uchaguzi katika kampuni ya watu kwani hamjui Bongo Movie ni ya watu kumi? Kwa maana hiyo asingedhulumiwa angekaa kimya.
Ni ukweli usiopingika kama Cloud angepata mgawo wake kiusahihi asingeongea na kuwashtua wengine kuwa kumbe wapo Bongo Movie kwa ajili ya watu wachache na si wasanii wote walioanzisha klabu hiyo.
JB na wenzako mnatakiwa muandae kikao cha dharura na kuzungumza ukweli na si kukimbilia kujiuzulu kwani hakutasaidia chochote katika kurudisha amani ndani ya Bongo Movie.
Mnatakiwa muueleze fedha zote mlizozipata zimefanyiwa nini? Kwa maelezo niliyoyapata ni kwamba fedha mlizolipwa baada ya kushiriki tamasha moja kubwa hapa nchini hamkuwafikishia wenzenu, mlipoona wanapiga kelele ndipo mlipojichangisha na kutoa milioni moja ili wagawane, huu ni ufisadi tena wa hali juu.
Ombeni radhi for the good of the game!


No comments:

Post a Comment