Thursday, November 29, 2012

WANAFUNZI MACHANGUDOA KATIKA CHUO KIKUU CHA DODOMA ( UDOM ) WAANZA KUSAKWA


RAIS wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOSO), Paul Yunge, amesema kuwa wanafanya uchunguzi wa kina ili kuwanasa wanafunzi wa chuo hicho wanaojihusisha na biashara ya kujiuza kimwili ili wawachukulie hatua.


Yunge alifafanua kuwa, wanafunzi watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo watachukuliwa hatua kali za kinidhamu ili iwe fundisho kwa wengine.


Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Yunge alisema kazi ya kufanya uchunguzi tayari imeanza na wanategemea wakati wowote watabaini ukweli kuhusiana na jambo hilo.


Alifafanua kuwa, wanafunzi wanaojihusisha na vitendo hivyo wanakidhalilisha na kukishushia heshima chuo hicho ambacho kimsingi kinapaswa kuwa kioo.


“Ni aibu sana kama watu wamekuja UDOM kusoma na badala yake wanageuka na kufanya biashara ya kujiuza ambayo ni ya kudhalilisha utu wao pamoja na chuo kwa ujumla. Jambo hili lazima tulifanyie kazi,” alisema.


Yunge alidai kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya taarifa hiyo kuripotiwa na vyombo vya habari, kitendo ambacho kimeisononesha nchi nzima ukiwemo uongozi wa chuo pamoja na wazazi wa wanafunzi hao.


Hatua ya serikali ya chuo kuanza uchunguzi imekuja baada ya baadhi ya vyombo vya habari wiki iliyopita kuripoti kuwa baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho wanajiuza katika sehemu mbalimbali za mji wa Dodoma.


No comments:

Post a Comment