Tuesday, May 21, 2013


MPANGILIO wa alama mpya za kufaulu kwa wahitimu wa kidato cha sita waliohitimu mwaka jana, ambao matokeo ya mitihani yao yanaweza kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa, unadaiwa kuzua aibu na kama si uamuzi uliotajwa bungeni wa matumizi ya alama za ufaulu za zamani, matokeo hayo yangeibua aibu kama ilivyojitokeza kwa kidato cha nne, 2012.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari kutoka Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) ambalo linaendelea kupanga matokeo hayo ya kidato cha sita kwa kuzingatia alama za zamani kama ambavyo taarifa ya awali ya Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ilivyosomwa bungeni hivi karibuni, hali ingekuwa mbaya zaidi katika ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha sita kiasi cha kuweza kutishia uhai wa vyuo vikuu nchini kukosa wanafunzi wa kutosha.

“Hali ilikuwa mbaya sana kama alama za kufaulu zingeachwa zitumike zile mpya na si za zamani. Vyuo vikuu nchini visingeweza kupata wanafunzi wa kutosha.

 "Tatizo hapa si uwezo wa wanafunzi moja kwa moja katika kumudu mitihani bali ni kufanywa kwa mabadiliko ya alama bila kuwaandaa.

" Alama hizi zilipaswa kuanza kutumika na wanafunzi wapya, yaani kama wanaanza kidato cha kwanza wawe wanapewa mitihani ya kupimwa kwa kuzingatia alama mpya na waendelee nazo hadi mitihano yao ya mwisho.

“Na hivyo hivyo kwa wanafunzi wa kidato cha sita. Alama hizi mpya zinapaswa kutumika kwako kuanzia wakiwa kidato cha tano mara wanapoanza shule, kila mitihani wanayopewa isahihishwe na kupangiwa alama kwa kutumia hizi alama mpya,” kinaeleza chanzo chetu cha habari kutoka NECTA.

Kwa mujibu wa mabadiliko hayo ya alama, alama mpya zilizokuwa zimetumika awali ni daraja F kuanzia 34 hadi sifuri; badala ya alama hiyo F kuanzia 20 hadi 0; daraja D kwa kuzingatia alama mpya linapaswa kuanzia 35 tofauti na awali, yaani alama 21.

Taarifa zaidi zinabainisha ya kuwa, kati ya sababu za kuchelewa kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha sita tofauti na muda uliotarajiwa yaani mwanzoni mwa Mei, ni pamoja na upangaji upya matokeo hayo, ikiwa ni tofauti na ilivyokuwa kwa kidato cha nne ambapo matokeo yalitangazwa na kisha kufutwa ili kuyapanga upya kwa kutumia alama za zamani.

Lakini alipoulizwa kuhusu masuala hayo ndani ya NECTA, Ofisa Habari wa Taasisi hiyo nyeti nchini, John Nchimbi alisema; “Kwa sasa niseme tu kwamba mchakato wa kuandaa matokeo ya kidato cha sita unaendelea, siwezi kusema lini hasa utakamilika lakini nina uhakika ni katika muda muafaka.”

Kuhusu matokeo ya kidato cha sita kucheleweshwa kutokana kupangwa upya ili kupunguza idadi ya waliofeli kutokana na matumizi ya alama mpya za kufaulu, Nchimbi anasema; “Unajua haya maagizo haya ya bungeni (kupanga matokeo kwa kuzingatia alama za zamani) yamekuja wakati mchakato wa kuandaa matokeo ulikwishaanza. Kwa hiyo baada ya maagizo ilibidi kufanya kazi hiyo tena kwa kufuata maagizo hayo.”

Hata hivyo, hakuweka bayana kama matokeo ya awali kabla ya maagizo ya Serikali yaliyotolewa bungeni kutumia alama za zamani yamewafanya wanafunzi wengi kufeli na badala yake akasema; “Hilo siwezi kulizungumzia kwa sababu mchakato wa matokeo hayo haukuwa umefika mwisho. Takwimu rasmi hazikuwa zimekamilishwa. Kwa hiyo si sahihi kusema rasmi walifeli.”

Lakini wakati hali ikiwa hivyo kwa upande wa matokeo yanayotarajiwa ya kidato cha sita, taarifa zaidi zinabainisha ya kuwa, baada agizo la serikali la kufuta na kurejewa upya kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012, takriban wanafunzi 50,000 wamepata unafuu katika matokeo yao tofauti na awali.

Awali, kwa kuzingatia matokeo ya kidato cha nne mwaka jana yaliyotangazwa Februari, mwaka huu jijini Dar es Salaam, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk. Shukuru Kawambwa, jumla ya watahiniwa 126,847 tu kati ya watahiniwa 397,136 waliofanya mtihani huo walifaulu.

Katika matokeo hayo idadi ya wasichana waliofaulu ilitajwa kuwa ni 46,181 wakati wavulana waliofaulu ikiwa wanafunzi 80,686 na idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu ni 16,112 kati yao watahiniwa 61,001 waliofanya mtihani wasichana ni 6,7751 na wavulana 9,361.

Katika matokeo hayo watahiniwa waliopata daraja la kwanza ni 1,641, daraja la pili 6,453 na daraja la tatu ni 15,426, wakati waliopata sifuri ni 240,903 lakini kwa kuzingatia taarifa za vyanzo vyetu ndani ya Baraza, idadi hiyo itabadilika kwa sababu ya alama kuongezwa kwa watahiniwa hao wa mwaka 2012.

Lakini matokeo hayo yalitangazwa pamoja na vituko walivyofanya baadhi ya wanafunzi, vikiwamo vituko vya kuandika matusi kwenye karatasi za majibu ya mitihani na kutokana na makosa hayo, watahiniwa 789 walifutiwa mitihiani yao.

No comments:

Post a Comment