Saturday, December 15, 2012

HII NDO BURUDANI YA KOFFI OLOMIDE PALE LEADERS CLUB

Kampuni ya bia ya Serengeti Breweries kupitia bia yake ya Tusker lager jumamosi jioni iliandaa tamasha maalumu kabisa la nyama choma pamoja na burudani ya muziki iliyopewa jina la Tusker Carnival na kumualika msanii nguli wa Kiafrika Koffi Olomide ambaye alikuja nchini maalumu katika tamasha hilo pamoja na kusherehekea kutimiza kwa miaka 13 kwa kituo cha Clouds Fm.


Tamasha hilo lilianza mapema mida ya alasiri ambapo wananchi kutoka maeneo mbali mbali ya jiji la Dar-es-Salaam na vitongoji vyake walikwenda katika viwanja vya Leaders Club kwa ajili ya kupata nyama choma huku wakishushia na bia yao pendwa ya Tusker Lager ambao ndio walikuwa wadhamini wakuu wa tukio hilo.

Aidha katika kulipamba na kulinogesha tamasha hilo bendi kadhaa za nyumbani ikiwemo Twanga Pepeta, Mapacha watatu, Diamond Musica na Skylight Band zilialikwa kutumbuiza na kuwapa raha mashabiki na wapenzi wa burudani ya Muziki wa Dansi nchini Tanzania.

Bendi zote zilifanya makamuzi ya nguvu, lakini ushindani mkali ulionekana kutoka kwa bendi ya Diaomond Muzica iliyokuwa ikongozwa nae Hassan Liver Sultan na Bendi ya Skylight ambayo iliongozwa na kina Joniko Flower ambapo mashabiki wengi waliofika katika viwanja vya Leaders walionekana kuzifurahia.

Ilifika zamu ya msanii mwalikwa wa tamasha hilo la Tusker Carnival Charles Antoine Koffi Olomide ambapo alipanda stejini majira ya saa sita za usiku na ushehee akitanguliwa na mwimbaji wake mahiri wa kike katika kundi la Quartier Latin bibie Cindy ambaye naye alikonga nyoyo za mashabiki wengi waliojitokeza jana kwa sauti nyororo, murua na ya kuvutia.

Koffi Olomide alidumu kwa takriban saa moja akiimba nyimbo zake nyingi zaidi kutoka albamu yake ya nyuma Affaire D’Etat kama Julia na kadhalika.


Koffi olomide alitumia wasaa wake wa kutumbuiza kuwashukuru watanzania kwa moyo wa upendo na ukarimu walionao kwake akisema amewapatia mashabiki wake wa Tanzania nafasi ndani ya moyo wake na pia aliwatambulisha washiriki wa kumsaka mrembo anayegombania taji la Miss East Africa jukwaani.

Jumapili Koffi Olomide na kundi zima la quartier Latin wapo katika uwanja wa CCM Mwanza kutumbuiza kwa wakazi wa kanda ya ziwa.
































 





No comments:

Post a Comment